Monrovia, Liberia
Mshambuliaji wa zamani wa PSG, AC Milan na timu ya taifa ya Liberia, George Weah amempongeza mpinzani wake Joseph Boakai baada ya kuibuka kinara katika kura za kiti cha urais wa Liberia.
Weah, 57, ambaye pia amewahi kutwaa tuzo ya Ballon d’Or na kutangazwa mwanasoka bora wa dunia wa Fifa mwaka 1995, alisema huu ni wakati sahihi wa kuacha ubinafsi na kuweka mbele maslahi ya taifa.
“Watu wa Liberia wamezungumza na tumeisikia sauti yao, lakini kwa namna ushindani ulivyokuwa wa karibu mno inaonesha jinsi wananchi walivyogawanyika katika makundi kwenye nchi yetu,” alisema Weah.
Weah aliwataka watu wa Liberia kujiponya kutokana na makundi hayo ambayo alisema yametokana na kampeni za uchaguzi na kuwakumbusha kusimama pamoja kama watu wa taifa moja.
Kwa sasa Weah hata hivyo ataendelea kuwa madarakani hadi Januari mwakani atakapomkabidhi rasmi Boakai kiti hicho.
Boakai mwenye umri wa miaka 78, alishindwa na Weah kwa tofauti kubwa ya kura katika uchaguzi wa mwaka 2017 kabla ya kuibuka kinara mwaka huu baada ya kufanya kampeni zilizowapa matumaini makubwa wapiga kura.
Marekani ilikuwa miongoni mwa zilizompongeza Boakai kwa kushinda kiti cha urais na kumpongeza Weah kwa kukubali matokea. “Tunawahimiza wananchi wote kufuata mfano wa Weah kwa kukubali matokeo,” ilieleza taarifa ya serikali ya Marekani.
