Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo amesema wamewaandalia kipigo cha aibu wapinzani wao Mtibwa Sugar katika mchezo wa raundi ya 10 wa Ligi Kuu NBC utakaochezwa Ijumaa, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Dabo alisema katika kipindi cha wiki mbili ambacho ligi ilisimama walikuwa wakifanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza na kucheza mechi za kirafiki ambazo ana imani zimewaweka tayari kwa mechi zinazowakabili.
“Mazoezi na mechi za kirafiki tulizocheza wakati wa mapumziko ya ligi yametuimarisha kuliko ilivyokuwa mwanzoni ndio manaa nimewatahadharisha Mtibwa Sugar wajiandae kwani kila mchezaji kwenye kikosi changu amekuwa bora kuliko tulivyoanza msimu,” alisema Dabo.
Kocha huyo raia wa Senegal alisema amefurahi kuona safu yake ya ushambuliaji ikifunga mabao mengi katika mechi za kirafiki lakini hata safu ya ulinzi imeimarika kwa kutoruhusu mabao kama ilivyokuwa mwanzoni.
Alisema lengo lake kubwa ni kuhakikisha wanamaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni ingawa si kitu rahisi kutokana na ubora walionao vinara Yanga lakini watapambana kuhakikisha wanafanikiwa.
Azam tayari imeshapoteza mechi mbili kati ya tisa ilizocheza na kwa sasa ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 19 sawa na Simba iliyo nafasi ya tatu na idadi kama hiyo ya pointi.
