Na mwandishi wetu
Timu ya Yanga imepania kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kuthibitisha hilo imejipanga kuhakikisha inapata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.
Hayo yamesemwa Jumanne hii na Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe wakati kundi la kwanza la wachezaji wa timu hiyo wakianza safari ya kuelekea Algeria kwa mchezo huo kabla ya kufuatiwa na kundi la pili Jumatano la wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa.
Kamwe alisema wanataka kufanya vizuri ili kufika mbali ambako hakuna timu ya Tanzania imewahi kufika kwenye michuano hiyo.
Katika hilo Kamwe alisema inawalazimu kupambana mno kwanza kwenye mechi za hatua ya makundi ili kufikia ndoto yao hiyo na kukata kiu za Wanayanga.
“Tunataka kufanya vizuri Ligi ya Mabingwa msimu huu na ndio kiu ya kila Mwanayanga, tunataka kufika katika hatua ambazo timu za Tanzania hazijawahi kufika na huwezi kufika kama hufanyi vizuri hatua ya makundi. Huu mchezo wa kwanza ugenini ni muhimu sababu unakupa nini tutegemee kwenye mchezo wa pili,” alisema Kamwe.
Alisema baada ya kumalizana na Belouizdad katika mchezo utakaochezwa Ijumaa hii mjini Algiers pia wanataka kuanza vyema mchezo utakaofuata dhidi ya Al Ahly wa Desemba 2, mwaka huu watakaokuwa nyumbani ili kutimiza malengo yao.
“Hata mchezo wa pili wa Dar es Salaam dhidi ya Al Ahly pia ni muhimu zaidi kwetu, ni mchezo wa kutafuta matokeo ya kwanza nyumbani, pointi za ugenini zinatafutwa kimkakati ila za nyumbani ni muhimu kuondoka nazo zote tisa ili kuweka mazingira bora ya kuvuka makundi,” alisema Kamwe.
Alisema, benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Miguel Gamondi limeandaa vizuri kikosi cha mapambano na wanashukuru mpaka sasa hawana majeruhi hata kwa wachezaji walio kwenye timu zao za taifa na wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kufahamu kama kutakuwa na majeraha yoyote, wayamalize mapema ili kuwa na jeshi kamili katika mechi za hatua hiyo.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu NBC wakishamalizana na Belouizdad na Al Ahly, Desemba 8, mwaka huu pia watakuwa ugenini kumaliza ungwe ya kwanza ya hatua ya makundi kwa kuumana na Medeama ya Ghana, Uwanja wa Baba Yara mjini Kumasi.
