Rio de Janeiro, Brazil
Mechi ya Brazil na Argentina ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 ambayo Argentina imeshinda kwa bao 1-0 imechelewa kuanza kwa dakika 30 baada ya kutokea vurugu za polisi na mashabiki.
Argentina katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Maracana ilipata bao hilo pekee kipindi cha pili lililofungwa na Nicolas Otamendi na kuifanya Brazil ipoteze kwa mara ya kwanza mechi ya kufuzu ikiwa katika uwanja wa nyumbani.
Vurugu hizo ziliibuka baada ya mashabiki wa Argentina na Brazil kuanza kupambana wakati nyimbo za taifa zikiimbwa hali iliyowafanya polisi kutumia virungu kukabiliana na mashabiki wa Argentina.
Mashabiki wa Argentina nao walijibu mapigo kwa kuwarushia polisi viti hali iliyofanya Uwanja wa Maracana kuwa kama sehemu ya vita baada ya mashabiki wengine kukimbilia katikati ya uwanja ili kukwepa vurugu.
Wakati mapambano hayo yakiendelea, shabiki mmoja aliyejeruhiwa alionekana akiwa amebebwa kwenye machele na kutolewa nje ya uwanja na maofisa wa huduma wa kwanza.
Baadhi ya wachezaji wa Argentina walionekana wakiwataka mashabiki waliokuwa jukwaani kutulia ingawa muda mchache baadaye nahodha wa timu hiyo, Lionel Messi aliwaongoza wenzake kurudi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Kipa wa Argentina, Emiliano MartÃnez alikimbia hadi karibu na mashabiki wa timu yake kwenye jukwaa huku akiwataka polisi kuhakikisha wanatuliza vurugu.
“Tuliwaona polisi wakipiga watu, na wachezaji wengi hapa ndugu zao wa familia wapo maeneo hayo, hatukuweza kuendelea kucheza mpira,” alisema Messi baada ya mechi hiyo.
Wachezaji wa Argentina inadaiwa waliwaambia wenzao wa Brazil kwamba wangerudi uwanjani baada ya hali kutulia na hatimaye walirudi baada ya dakika 22 na kufanya mazoezi mepesi kwa dakika kama nne kabla ya mechi kuanza.
“Tuliamua kuondoka uwanjani kwa sababu haingewezekana kucheza mpira katika mazingira kama yale, na pia tulidhani kwa sisi kwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ingesaidia kutuliza hali,” alisema Messi.
Wakati mechi ikianza kundi kubwa la polisi liliwazingira mashabiki wa Argentina waliokuwa wakishangilia, polisi hao walikuwa wakiwadhibiti mashabiki hao katika eneo ambalo lilikuwa na mashabiki wapatao 3,000.
Tiketi zote 69,000 za mechi hiyo ziliuzwa, mashabiki wa Brazil ambao walionekana wakimzomea na wakati mwingine kumshangilia Messi kabla ya kuanza kwa vurugu, baada ya mechi kuanza walianza kuimba nyimbo za kumsakama.
“Timu hii inaendelea kuweka historia, ushindi mkubwa kwenye dimba la Maracana ingawa umekutana na vipigo kwa mashabiki wa Argentina kwa mara nyingine katika mechi dhidi ya Brazil, ukichaa huu hauwezi kuvumiliwa, na lazima uachwe sasa,” alisema Messi
