Rio de Janeiro, Brazil
Mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Vinicius Junior amezindua kampeni kwa ajili ya kukabiliana na matukio ya ubaguzi wa rangi.
Vinícius amekuwa mlengwa wa mara kwa mara wa matukio ya ubaguzi wa rangi katika mechi za La Liga na sasa ameamua kuanzisha kampeni hizo kwao Brazil akihusisha matukio mbalimbali yenye lengo la kutoa ujumbe wa kukataa ubaguzi wa rangi.
Bango kubwa lenye picha ya Vinícius likiwa na maandishi ‘Racism, don’t pretend you don’t see it’ yaani ubaguzi wa rangi usijifanye huoni’, yameonekana katika miji karibu yote mikubwa nchini Brazil.
Sambamba na hilo, Vinícius pia amekuwa akitumia mitandao ya kijamii ya Twitter au X na Instagram kusambaza taarifa mbalimbali, katika Instagram ana ujumbe unaosomeka, “huu ndio ujumbe wangu, ni leo na siku zote.”
Oktoba mwaka huu Vinícius alipewa tuzo ya Socrates ikiwa ni heshima kwake kwa namna ambavyo amekuwa akijitoa katika shughuli za kibinadamu nchini Brazil.
“Inakera kwa wakati wote kulazimika kuzungumzia ubaguzi wa rangi lakini nimejiandaa kwa hilo, kwa wakati wote kuwa tayari kuzungumza inapolazimu kufanya hivyo ili kila mtu abaki kuwa imara kwa sababu nitawapigania, inasikitisha nazungumzia ubaguzi wa rangi maisha yangu yote, ningependa niwe mwenye kuzungumzia soka,” alisema Vinicius.
Vinicius inadaiwa aliandaa fulana 5,000 zenye maandishi ya kupiga vita ubaguzi wa rangi ambazo zilitarajiwa kugaiwa kwa mashabiki kwenye mechi ya jana Jumanne ya kufuzu Kombe la Dunia kati ya Brazil na Argentina lakini mpango huo ulifutwa dakika za mwisho.
