Na mwandishi wetu
Timu ya Taifa ya Morocco imeanza kufifisha ndoto za timu ya Tanzania ya Taifa Stars kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa Jumanne hii usiku kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Morocco au Atlas Lions waliandika bao la kwanza katika dakika ya 27 ya mchezo huo lililofungwa kwa shuti la mbali na Hakim Ziyech na mpira kumshinda mlinda mlango wa Stars.
Dakika 10 baada ya kuanza kipindi cha pili, juhudi za Morocco kulisakama lango la Stars zilizaa matunda baada ya beki wa Azam FC Lusajo Mwaikenda kuizawadia timu hiyo bao la kujifunga.
Mambo yaliendelea kuiharibikia Stars dakika nyingine 10 baada ya bao hilo walipojikuta wakibaki 10 uwanjani baada ya beki wa kushoto Novatus Dismas anayekipiga Shakhtar Donetsk ya Ukraine kulimwa kadi ya pili ya njano na hivyo kuwa nyekundu.
Kipigo hicho kinaiweka Stars pabaya baada ya kuanza na ushindi wa bao 1-0 katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Niger, matokeo ambayo yaliibua matumaini kabla ya mechi ya Morocco kufifisha matumaini hayo.
Mambo yangeweza kuwaharibikia zaidi Stars kama si beki wa Morocco anayekipiga PSG, Achraf Hakimi kukosa penalti mapema dakika ya tatu ya mchezo huo.
Mbali na Morocco na Niger, timu nyingine zilizo Kundi E pamoja na Stars ni Zambia, Congo Brazaville na Eritrea ambayo hata hivyo imejitoa katika michuano hiyo.
Zambia ilianza na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Congo lakini nayo imakwama katika mechi yake ya pili baada ya kulala kwa mabao 2-1 mbele ya Niger.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zimepangwa kufanyika katika nchi tatu za Mexico, Canada pamoja na Marekani.
Kimataifa Morocco yaichapa Stars 2-0
Morocco yaichapa Stars 2-0
Read also