New York, Marekani
Moja ya jezi sita alizovaa mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 inaandaliwa utaratibu wa kuuwa kupitia mnada maalum.
Messi, 36, aliiongoza vyema Argentina katika fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar hadi kubeba taji hilo kwa kuwabwaga mabingwa watetezi Ufaransa kwenye mikwaju ya penalti.
Katika orodha ya jezi zinazotarajia kupigwa mnada, imo jezi ambayo mchezaji huyo aliivaa katika mechi ya fainali huku matarajio yakiwa ni kukusanya zaidi ya Pauni 8 milioni kupitia mnada huo ambao utafanyika jijini New York ukisimamiwa na taasisi ya Sotheby.
Jezi ambayo hadi sasa imeweka rekodi ya kuuzwa bei mbaya ni ile ambayo aliivaa Diego Maradona wa Argentina mwaka 1986 katika mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya England na kufunga bao la mkono.
Jezi hiyo ambayo ilibatizwa jina la ‘hand of god jersey’ iliuzwa mwaka 2022 kwenye mnada kwa Pauni 7.1 milioni.
Msimamizi mkuu wa mnada huo, Brahm Wachter kutoka Sotheby alisema kwamba kuuzwa kwa mnada jezi za Messi kutakuwa tukio kubwa na la kihistoria katika minada.
“Fainali za Kombe la Dunia 2022 zinabaki kuwa moja ya matukio makubwa ya kihistoria kwenye michezo yakiunganishwa na safari ya aina yake ya Messi ambaye kwa ujasiri amefanikiwa kudhihirisha hadhi yake ya kuwa mchezaji bora wa wakati wote,” alisema Wachter.
Jezi ya Messi itawekwa sehemu ya wazi kwa kila mtu kuiona wakati wote ambao taratibu za mnada zitakuwa zikiendelea kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 14.