London, England
Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate amewataka wachezaji wake kupambana ili wawe namba moja kwa ubora duniani kupitia takwimu zinazotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Kwa sasa England inashika namba nne kwa ubora na leo Jumatatu jioni itaumana na Macedonia, mechi ambayo ni ya mwisho katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024.
Timu hiyo hata hivyo tayari imeshafuzu fainali hizo zitakazofanyika nchini Ujerumani Juni mwakani na matokeo ya sare na Macedonia yanatosha kuihakikishia timu hiyo kumaliza ikiwa kundi la timu vinara.
“Kama unakuwa timu namba moja maana yake ni kwamba hakuna nafasi ya kuzembea au kuchukulia mambo kirahisirahisi, kama tutakuwa namba moja basi hata kiwango cha uchezaji kinatakiwa kuwa juu kila wakati,” alisema Southgate.
Argentina, mabingwa wa Kombe la Dunia kwa sasa ndio wanaoshika namba moja duniani wakifuatiwa na Ufaransa inayoshika nafasi ya pili na Brazil ni ya tatu wakati England imeendelea kuwa katika tano bora kwa miaka mitano mfululizo.
Katika takwimu zinazotarajiwa kutolewa Novemba 30 mwaka huu na Fifa, England inatarajiwa kuipiku Brazil na kushika nafasi ya tatu lakini kwa Southate hilo halitoshi, anachotaka ni kuiona timu hiyo katika nafasi ya kwanza.
“Je nina mtazamo wa kuwa namba moja? Jibu ni ndio kwa sababu mwishowe unafanikisha hilo kwa kushinda kila mara na pia unatakiwa kucheza vizuri kwenye mashindano kwani pointi za kukupandisha zinakuwa juu kupitia mashindano,” alisema Southgate.
Southgate pia alisema kwamba, kuwa namba moja pia kunaweka malengo bora ya kila siku kuanzia kwenye uwanja wa mazoezi hadi nje ya uwanja wa mazoezi.
“Baada ya mechi iliyo mbele yetu tunaweza kuwa namba tatu duniani lakini bado tuna nafasi mbili kufika tunapopataka, kwa hiyo hatuwezi kupoteza mchezo,” alisema Southgate.
