Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa timu ya Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge amekiri kuvutiwa na kiwango cha kiungo wa KMC, Awesu Awesu (pichani) na amepanga kuwaarifu viongozi wake ili kumuongeza kwenye kikosi chake.
Juzi Al Hilal ilicheza mechi ya kirafiki na KMC ikiwa ni mchezo wa kujiandaa na mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Licha ya mchezo huo kuisha kwa sare ya bao 1-1, kocha huyo alisema mchezo huo umesaidia kujua mapungufu yaliyopo kwenye kikosi chake lakini kingine cha msingi amevutiwa na uwezo uliooneshwa na Awesu.
“Kwa kipaji chake nilitarajia kumuona akicheza Simba, Yanga au Azam lakini yupo KMC, najua ndio mambo ya mpira yalivyo lakini nimevutiwa na uwezo wake na nitakutana na uongozi wangu kuona kama tunaweza kumpata,” alisema Ibenge.
Kocha huyo alisema katika mchezo huo Awesu ndiyo mchezaji aliyeisumbua zaidi timu yake kutokana na uwezo na akili kubwa aliyokuwa nayo katika kusambaza mipira kwa washambuliaji wake kitu ambacho kilimlazimisha kumwekea mtu maalumu wa kumdhibiti.
Awesu yupo KMC kwa mkopo akitokea Azam FC, ambako aliondolewa baada ya kushindwa kupigania namba na viungo wengine kama Sospeter Bajana, James Akaminko, Yahya Zaid na Feisal Salum.
