Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Adel Amrouche amesema ana imani kubwa na vijana wake kufanya vizuri katika mchezo wa kesho Jumanne dhidi ya Morocco utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Stars inashuka katika mchezo huo wa pili wa Kundi E wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya juzi Jumamosi kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Niger.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Amrouche alisema wanaenda kucheza na timu kubwa na ana imani ya kufanya vizuri katika uwanja wa nyumbani.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu, nina imani na vijana wangu wana uwezo wa kupambana na kupata matokeo mazuri katika mchezo wetu wa kesho dhidi ya Morocco,” alisema Amrouche.
“Hata ukiangalia katika viwango vya soka tunaona jinsi Tanzania ilipo, lakini pia timu ya taifa hatuna muda mwingi wa kukaa na wachezaji, tunalazimika kujiandaa kulingana na mechi iliyopo mbele yetu,” alisema Amrouche.
Amrouche aliongeza kuwa mechi wanayoenda kucheza ni kubwa na ngumu ambayo itaonyesha ushindi mkubwa kwa sababu ya ukubwa wa wapinzani ambao wanakutana nao.
Naye kocha mkuu wa Morocco, Walid Regragui alisema anafurahi kufika Tanzania salama na wako tayari kwa ajili ya kusaka ushindi katika mchezo huo kwa kuwa wamedhamiria kufanya vizuri tangu katika mechi za kwanza za kuwania kufuzu katika michuano hiyo mikubwa duniani.
“Ili mtu afuzu basi mechi ya kesho ni muhimu kuhakikisha tunapata ushindi, tunaenda kucheza mechi kwa umakini mkubwa, hatuwezi kuangalia tunacheza na timu ya aina gani,” alisema Regragui.
“Tanzania hatuwachukulii kama wako daraja la chini, tunawaheshimu na wanajituma sana na ukizingatia wanacheza mbele ya mashabiki wao watapambana kwa ajili ya kupata matokeo mazuri,” alisema Regragui.
Stars inashuka kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu kupata ushindi dhidi ya Morocco kwenye Uwanja wa Mkapa, mtanange uliopigwa mwaka 2013 ambapo Stars iliibuka na ushindi wa mabao 3-1. Mbwana Samata alifunga mawili na jingine lilifungwa Thomas Ulimwengu.
