London, England
Klabu ya Everton imenyang’anywa pointi 10 katika Ligi Kuu England (EPL) baada ya kukutwa na hatia ya kuvunja kanuni ya ligi hiyo inayohusu faida, adhabu inayoishusha timu hiyo hadi nafasi ya 19.
Adhabu hiyo kubwa katika historia ya EPL inaiweka klabu hiyo mahali pagumu kwani sasa inakuwa imebakiwa na pointi nne tu katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 20.
Mara baada ya kutangazwa adhabu hiyo, Everton walieleza kushtushwa na adhabu waliyoiita kuwa ni kubwa, isiyo na uhalali na ambayo si haki na klabu hiyo inajipanga kuikatia rufaa.
Machi mwaka huu, tume huru ilikabidhiwa jukumu la kushughulikia suala la klabu hiyo na ingawa uamuzi umefikiwa wa kuinyang’anya pointi 10 lakini haikuwekwa wazi kwa undani ni kanuni ipi hasa iliyovunjwa na klabu hiyo.
Everton ilitoa taarifa yake Machi mwaka huu ikieleza kupata hasara kwa mwaka wa tano mfululizo baada ya kuonesha katika taarifa hiyo kuwa ilikuwa na hasara iliyofikia Pauni 4.7 milioni katika mwaka wa fedha wa 2021-22.
Klabu za EPL zinaruhusiwa kuwa na nakisi ya Pauni 105 milioni kwa kipindi cha miaka mitatu na Everton ilikiri kwenda kinyume na kanuni inayohusu faida ya klabu katika kipindi kilichoishia mwaka 2021-22.
Baada ya suala hilo kusikilizwa kwa siku tano tume huru iliyopewa jukumu hilo ilihitimisha kuwa hasara ambayo Everton iliipata katika kipindi hicho ilifikia Pauni 124.5 milioni.
Kimataifa Everton yapokwa pointi 10 EPL
Everton yapokwa pointi 10 EPL
Read also
