Na mwandishi wetu
Kiungo wa timu ya Yanga, Khalid Aucho amefungiwa kucheza mechi tatu pamoja na kutozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union, Ibrahim Ajib.
Adhabu hiyo imetangazwa Ijumaa hii na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ikifafanua kuwa mchezaji huyo alifanya kosa hilo katika mechi ya Ligi Kuu NBC kati ya Yanga na Coastal iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Katika mechi hiyo hiyo, Coastal iliyokuwa mwenyeji wa mchezo imetozwa faini ya Sh 1,000,000 kwa kosa la wachezaji wake kuchelewa kutoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kusababisha kuchelewa kuanza mchezo huo kipindi cha kwanza na cha pili.
Mwingine aliyekutana na rungu la bodi hiyo ni mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo, Emmanuel Mwandembwa wa Arusha ambaye amefungiwa miezi sita kwa kushindwa kutafsiri sheria 17 za soka na kumfanya ashindwe kuumudu vyema mchezo huo.
Wakati huo huo klabu za Simba na Yanga zimetozwa faini tofauti tofauti, Yanga imetozwa faini ya Sh milioni tano kwa kosa la kutumia mlango usio rasmi, tukio ambalo pia lilitokea katika mechi yao dhidi ya Simba.
Katika mechi hiyo hiyo iliyopigwa Novemba 5 mwaka huu na ambayo Simba ililala kwa mabao 5-1, timu hiyo pia imetozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la wachezaji wake kuchelewa kutoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Wengine waliokumbana na rungu la bodi hiyo na kutozwa faini ya Sh 500,000 kila mmoja ni pamoja na mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis kwa kosa la kushangilia bao pekee alilofunga katika mechi hiyo mbele ya mashabiki wa Yanga na kuwaonesha ishara ya kuwafunga midomo.
Adhabu hiyo pia amepewa Henock Inonga wa Simba kwa kosa kama la Kibu pamoja na kipa wa Yanga, Djigui Diarra naye ilimkuta adhabu kama hiyo kwa kosa la kushangilia mbele ya benchi la ufundi la klabu ya Simba.
Kocha msaidizi wa Yanga, Mousa Ndiao naye ilimkuta adhabu kama hiyo kwa kilichodaiwa kuwa ni kuwatolea lugha ya matusi benchi la ufundi la Simba.
Soka Aucho afungiwa mechi tatu
Aucho afungiwa mechi tatu
Read also
