London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta ameingia matatani na huenda akaadhibiwa na Chama cha Soka England (FA) kwa kauli aliyoitoa baada ya timu yake kufungwa bao 1-0 na Newcastle katika mechi ya Ligi Kuu England.
Baada ya mechi hiyo, Arteta akionekana mwenye hasira alisema kwamba uamuzi uliofikiwa baada ya kurejea kwenye VAR na kuipa Newcastle bao ni aibu na fedheha katika ligi kuu.
Bao hilo lililofungwa na Anthony Gordon lilikubaliwa baada ya VAR kupitiwa mara tatu na kwa mara zote hizo iliyopewa ushindi ni Newcastle jambo lililomkera Arteta na sasa amepewa hadi Jumanne awe amejibu madai ya FA.
“Kauli za kocha huyo zimekwenda kinyume na taratibu kwa kuwakashifu waamuzi jambo linalouweka mchezo wa soka katika hali ya hatari,” ilieleza taarifa ya FA.
Taarifa ya klabu ya Arsenal ilimuunga mkono Arteta kwa madai kwamba ni jukumu la kocha kuitetea klabu na jinsi uamuzi ulivyokuwa ni jambo lisilokubalika hasa kwa kuwa makocha, wachezaji na mashabiki wote wanahitaji ubora.
Kipigo hicho kiliifanya Arsenal kuharibu rekodi yake ya kutopoteza mechi tangu kuanza kwa ligi hiyo msimu huu na timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya tatu ikiwa imezidiwa na vinara Man City kwa pointi moja.
