Na mwandishi wetu
Yanga SC imetinga hatua ya tano bora katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya Klabu Bora Afrika ambazo zinaandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Timu nyingine zilizoungana na Yanga katika hatua hiyo ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri, USM Algers ya Algeria, Wydad AC na mabingwa wa michuano ya African Football League, Mamelodi Sundowns.
Akizungumzia hilo Rais wa Yanga, Hersi Said alisema hiyo imetokana na uwekezaji pamoja na imani waliyoiweka katika mashindano ya kimataifa ikiwemo kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.
“Hatujafika hapa kwa bahati, uongozi tulipambana kusajili wachezaji wenye ubora na hatimaye tukapata matokeo mazuri, hilo tumeliendeleza msimu huu kwa kuongeza wachezaji wenye viwango na uzoefu wa mashindano haya leo tupo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Hersi.
Kiongozi huyo alisema kufika tano bora ya kinyang’anyiro hicho mwaka 2023 kwao ni mafanikio makubwa kwani kabla ya hapo kulikuwa na klabu 10 na zenye majina makubwa lakini hazijafika hatua hiyo.
Wakati huo huo, kipa wa Yanga, Djigui Diarra ameshindwa kupenya kwenye tano bora ya kuwania Tuzo ya Kipa Bora huku majina matano yaliyobaki yakiwa ni Mohamed El Shenawy wa Al Ahly, Yassine Bounou (Al Hilal), Andre Onana (Manchester United), Ronwen Williams (Mamelodi) na Edouard Mendy (Al-Ahli).
Pia, kupitia taarifa hiyo iliyotolewa leo Ijumaa na mtandao wa Caf imeonesha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ nayo imeshindwa kupenya kwenye timu tano bora zilizosalia kwenye Tuzo ya Timu Bora ya Taifa. Zilizotinga tano bora ni Gambia, Guinea ya Ikweta, Mauritania, Morocco na Senegal.
Hafla ya tuzo hizo inatarajiwa kufanyika Desemba 11, mwaka huu jijini Marakesh, Morocco.
