Bogota, Colombia
Siku chache baada ya Manuel Diaz kuachiwa na watekaji, hatimye amemshuhudia mwanaye Luis Diaz akifunga mabao mawili na kuiwezesha Colombia kuichapa Brazil 2-1, tukio lililomtoa machozi mzee huyo akiwa jukwaani.
Mechi hiyo ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 imekuwa ya kipekee kwa mzee huyo aliyetekwa Oktoba 28 na kujikuta akitokwa machozi ya furaha kama vile kutoamini kilichotokea.
Mzee huyo alijiangusha mbele ya watu waliokuwa karibu yake katika jukwaa moja la Uwanja wa Metropolitan na kuanza kushangilia pembeni ya mkewe Cilenis Marulanda huku akitokwa na machozi.
Tukio la kutekwa mzee huyo lilitokea kwenye kituo kimoja cha mafuta baada ya wanaume wawili waliokuwa kwenye pikipiki kumteka na mkewe na kukaa na mzee huyo kwa siku 12 ingawa mkewe aliachiwa muda mfupi baadaye.

Mzee huyo aliungana na familia yake kwa mara ya kwanza Jumanne iliyopita na mtoto wake Luis Diaz ambaye ni mchezaji wa Liverpool, akiwa Colombia kwa maandalizi ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia alipata nafasi ya kukutana na baba yake kwa mara ya kwanza tangu kutekwa kwa mzee huyo.
“Namshuruku Mungu, amefanya lililowezekana, kwa wakati wote tumeishi katika kipindi kigumu lakini maisha yanakufanya kuwa imara na jasiri, ni hivyo, ni soka ni maisha, tulikuwa na haki ya kupata ushindi,” alisema Luis Diaz mara baada ya mechi hiyo.
Katika mechi hiyo iliyopigwa jana Alhamisi, DÃaz alifunga mabao yote kwa kichwa katika dakika za 75 na 79 na kuipa timu ya Colombia ushindi wa kwanza dhidi ya Brazil katika mechi 15 za kufuzu Kombe la Dunia.