Na mwandishi wetu
Wachezaji wote wanaocheza soka nje ya nchi walioitwa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ wamesharipoti huku timu hiyo ikitarajiwa kuondoka kesho Alhamisi kwenda Marrakesh, Morocco kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Niger utakaochezwa Jumamosi.
Stars inaondoka na ndege iliyotolewa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na itarejea Novemba 19, mwaka huu baada ya mchezo huo ili kuja kuumana na Morocco Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Novemba 21, mwaka huu.
Wachezaji wanaocheza nje ni Mbwana Samatta, Himid Mao, Charles M’muobwa, Novatus Miroshi, Kwesi Kawawa, Abdi Banda, Morice Abraham, Haji Mnoga, Ben Starkie, Simon Msuva, Baraka Majogoro, Omary Mvungi na Ibrahim Joshua.
Ofisa habari wa TFF, Cliford Ndimbo alisema maandalizi yanaendelea vizuri na baada ya kukabidhiwa majina ya watakaosafiri na benchi la ufundi ataujulisha umma.
“Safari ndio inashughulikiwa muda wa kuondoka bado hawajasema, idadi ya wachezaji wanaosafiri nitathibitisha baada ya kuwa iko tayari baada ya sasa kuripoti kwa wachezaji wote wanaocheza nje ya nchi,” alisema Ndimbo.
Naye beki Himid Mao alisema maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji wote wana ari na mtu hawezi kuona tofauti ya wachezaji wageni na wazoefu kwa sababu wote wanafanya vizuri.
“Michezo miwili haitakuwa mepesi hasa mchezo wa ufunguzi dhidi ya Niger kwa sababu tunajuana, tumekutana kwenye michezo ya kufuzu AFCON. Mchezo na Morocco tunajua ni timu kubwa tunawaheshimu lakini kwa wachezaji tulionao na kocha naamini tutapata matokeo mazuri,” alisema Mao.
