Na mwandishi wetu
Timu ya Simba SC imerejea kuanza mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Icory Coast.
Wekundu hao walikuwa mapumziko tangu walipomaliza mechi yao ya Novemba 9, mwaka huu dhidi ya Namungo iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 kabla ya kurejea juzi kuanza mazoezi ya gym na kunyoosha misuli kabla ya kwenda kwenye mazoezi ya uwanjani.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa wachezaji walioingia kambini ni wale ambao hawakuitwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa kwa ajili ya mechi za timu za taifa za kalenda ya Fifa.
“Wachezaji walipewa mapumziko baada ya mechi yetu ya mwisho ya ligi dhidi ya Namungo na wamerejea mazoezini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mechi zetu za Ligi ya Mabingwa tukianza na Asec Mimosas, hivyo kikosi kimeanza rasmi kujipanga kwa ajili ya mechi hizo,” alisema Ally.
Simba inatarajia kuumana na ASEC Novemba 25 katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kupepetana na Jwaneng Galaxy ya Botswana Desemba 2 ikiwa ugenini.
Baada ya hapo Desemba 9, timu hiyo itakuwa ugenini jijini Casablanca, Morocco kuvaana na Wydad AC ya Morocco katika mechi ya kukamilisha hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Afrika.
