Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa zamani Simba SC, Ismael Aden Rage amewaeleza viongozi wa timu hiyo kuwa pamoja na tafrani inayoendelea kwa sasa katika klabu hiyo lakini wao pekee ndio wenye jukumu la kuweka mambo sawa.
Akifafanua zaidi Rage alisema kwamba viongozi hao ndio wenye jukumu la kuhakikisha Simba inabaki kwenye ubora wake kuelekea michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Rage ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Bodi ya Baraza la Ushauri Simba, alizungumza hayo alipokuwa akihojiwa na kituo cha luninga nchini zikiwa zimesalia takriban siku 10 kabla ya kuanza kwa hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Kiongozi huyo ameyasema hayo baada ya timu hiyo wiki iliyopita kufungwa mabao 5-1 na Yanga kisha kuondoshwa kwa kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ huku baadhi ya mashabiki wao wakishinikiza kujiuzulu kwa baadhi ya viongozi akiwemo Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu.
“Pamoja na yote, mpira sasa hivi uko kwa viongozi wa Simba, wao wana uwezo mkubwa wa kurudisha amani, upendo katika klabu yetu, sababu muda uliobaki sio mkubwa sana kuelekea Ligi ya Mabingwa, kwanza viongozi wetu wabadilike wawe wepesi kuongea na media, sio kila jambo wanamtegemea msemaji wetu wa klabu…
“Kuna mambo mazito ambayo msemaji hatakiwi kusema, anasema mwenyewe. Ni kama vile msemaji wa serikali, kuna mambo hawezi kuyaongea, anazungumza waziri mkuu, makamu wa rais au rais mwenyewe,” alisema Rage.
“Mfano baada ya kupigwa bao tano, lazima ukubali kwamba mabao matano kwa Simba yalikuwa ni mengi, tangu jina la Simba lianzishwe hatujawahi kufungwa mabao matano na Yanga na hiyo wameweka rekodi ya kutufunga tano kwa mara ya kwanza,” alifafanua Rage.
Mbunge huyo wa zamani wa Tabora Mjini pia amewashauri Yanga kutumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani ili kuwafunga wapinzani tishio katika Kundi D, Al Ahly ya Misri anayoieleza kupungua mno makali yake katika miaka ya hivi karibuni.
“Kwanza Ahly wanaweza kuwadharau Yanga kwa kujua timu kubwa huku ni Simba pekee, kwa hiyo Yanga kuna nafasi hiyo kwamba watacheza na timu ambayo inaweza ikawadharau na wao wakatumia nafasi hiyo, halafu hawa Ahly sasa hivi sioni kama ni tishio tena kama ilivyokuwa zamani wanatufunga tano tano, sasa hivi tunawafunga sisi wao ndio wanakomboa,” alisema.
Aliwataka pia siku ya mechi hiyo, Yanga ihakikishe inaujaza uwanja huku wakitumia ipasavyo sheria ya wenyeji kuchagua muda wa mechi na kuiweka iwe saa 10 jioni ili kuwapa shida Ahly kwenye mazingira ya joto na kuhakikisha wanapata ushindi mnono siku hiyo.
Hata hivyo katika mechi ya kwanza, Yanga itaanza dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria ugenini wakati Simba iliyo Kundi B, itaanza kwa kupepetana na ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
