London, England
Mchezaji wa Liverpool, Luis Diaz ambaye baba yake Manuel Diaz ametekwa na waasi wa Colombia ameifungia bao timu yake na baada ya bao hilo akaonesha fulana yenye maandishi ya kuwataka waasi wamuachie huru baba yake.
Diaz, 26, alifunga bao hilo jana Jumapili katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya Luton na kuiwezesha Liverpool kutoka sare ya bao 1-1.
Fulana ya ndani aliyovaa Diaz ilionesha maandishi yaliyosomeka ‘freedom for papa’ akihimiza kuachiwa huru kwa baba yake ambaye ametekwa na kundi la waasi nchini Colombia la ELN tangu Oktoba 28 mwaka huu.
“Mama yangu, kaka zangu na mimi tuna shauku kubwa, tuna mawazo na hatuna neno la kuelezea hisia zetu, maumivu yataisha pale tu tutakapokuwa naye pamoja nyumbani,” alisema Luis Diaz.
“Nawaomba wamuachie haraka, waheshimu utu wake na kuyamaliza maumivu haya ya kusubiri, tunawaomba wafikirie mara mbili matendo yake na kumuacha awe pamoja nasi,” alisema Luis Diaz.
Serikali ya Colombia imeendelea na msako unaohusisha wanajeshi na polisi kwa lengo la kumtafuta baba wa Luis Diaz na kutangaza donge nono kwa atakayefanikisha upatikanaji wa mzee huyo.
Baba wa Luis alitekwa na waasi waliokuwa kwenye pikipiki wakiwa na silaha wakati akiwa na mkewe kwenye kituo kimoja cha mafuta ingawa baadaye mkewe alipatikana.
