Na mwandishi wetu
Yanga imeifanyia unyama Simba kwa kuichapa mabao 5-1 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku Maxi Nzengeli akifunga mabao mawili kati ya hayo..
Ushindi huo maarufu ‘mkono’ au 5G unaifanya Yanga kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 21 na kuiacha Simba kwa tofauti ya pointi tatu ingawa Yanga imeizidi Simba mchezo mmoja na timu zote hizo kila moja imepoteza mechi moja.
Matokeo hayo pia yanavuruga rekodi ya kutopoteza hata mechi moja katika Ligi Kuu NBC aliyokuwa akijivunia kocha wa Simba, Roberto Olivieira ‘Robertinho’ badala yake sasa anakuwa amepoteza mchezo wa kwanza.
Ikimtumia kwa mara ya kwanza kipa wake namba moja, Aishi Manula aliyekuwa majeruhi kwa zaidi ya miezi sita, mapema dakika ya tatu Simba ilifungwa bao la kwanza mfungaji akiwa ni Kennedy Musonda ambaye aliujaza mpira wavuni kwa kichwa akiitumia krosi ya Yao Kouasi.
Iliwachukua dakika sita Simba kusawazisha bao hilo mfungaji akiwa Kibu Dennis ambaye kama Musonda naye aliujaza mpira wavuni kwa kichwa akiitumia pasi ya Saido Ntibazonkiza na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare.
Mambo yalianza kuwaharibia Simba dakika ya 64 waliporuhusu nyavu zao kitikiswa kwa mara ya pili kwa bao la Maxi Nzengeli akiitumia vizuri pasi ya Aziz Ki.
Dakika ya 73 safu ya kiungo na ulinzi ya Simba ikionekana kuyumba iliruhusu bao la tatu lililofungwa na Aziz Ki kabla Nzengeli hajaongeza bao la nne kwa Yanga na la pili kwake kwenye mechi hiyo katika dakika ya 77.
Karamu ya mabao ya Yanga ilihitimiswha na Pacome Zouzoua kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 87 baada ya beki wa Simba Henock Inonga kumchezea Maxi Nzengeli rafu ndani ya boksi na mwamuzi Ahmed Arajiga kuamuru ipigwe penalti.
Soka Yanga yaipiga Simba mkono
Yanga yaipiga Simba mkono
Read also
