Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Moses Basena amesema kuwa hawatarudia makosa ya mchezo uliopita yaliyosababisha wakapata sare na kuwaharibia hesabu zao.
Ihefu wanashuka dimbani kesho Jumamosi kuikabili Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu NBC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbeya.
Vijana wa Basena wanaoshika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi wanashuka kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupata sare ya mabao 2-2 na Singida Fountain Gate wakati Azam inayoshika nafasi ya tatu ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Mashujaa.
“Mchezo huu una maana kubwa kwetu, tunatakiwa kushinda ili kurejesha hali ya kujiamini kikosini baada ya morali yetu kushuka lakini tunarudi kurekebisha makosa yetu ili tukusanye pointi tatu kwenye mchezo ulio mbele yetu,” alisema Basena.
Kocha Msaidizi wa Azam, Bruno Ferry alisema baada ya kupata pointi tatu kwenye mchezo uliopita nguvu zao wanahamishia kwenye mechi ya Ihefu ingawa anaamini watakutana na upinzani mkubwa kwa kuwa watakuwa ugenini.
“Naamini utakuwa mchezo mgumu, wapinzani wetu wanapambana kupata matokeo lakini lengo letu ni kushinda kila mchezo ulio mbele yetu ili tuendelee kusogea juu ya msimamo wa ligi,” alisema Ferry.