
Nyota wa zamani wa mpira wa kikapu, Magic Johnson ametangazwa na jarida maarufu duniani la uchumi na biashara, Forbes kuwa bilionea na hivyo kufanya idadi ya wanamichezo mabilionea nchini Marekani kufikia wanne. Kwa kufikia hadhi hiyo, Magic Johnson sasa anakuwa katika kundi moja na wanamichezo wengine, Michael Jordan na LeBron James ambao ni wa mpira wa kikapu na Tiger Woods wa golfu. Tathmini ya Forbes inaonesha kuwa Magic Johnson ambaye amewekeza katika timu ya mpira wa kikapu na biashara nyinginezo ikiwamo viwanda ana utajiri unaofikia Dola bilioni 1.2. Katika misimu 13 aliyocheza mpira wa kikapu akiwa na timu ya Los Angeles Lakers katika ligi ya NBA nchini Marekani, Magic Johnson aliingiza dola 40 milioni lakini mambo yalianza kumbadilikia taratibu alipokutana na watu wa biashara na pato lake kuongezeka. Miongoni mwa utajiri wa Magic Johnson ni umiliki wake wa asilimia 60 katika kampuni ya bima ya maisha ambapo pato lake la mwaka kwa mujibu wa Forbes linatajwa kufikia takriban dola bilioni 2.6.
