Manchester, England
Kocha Erik ten Hag wa Man United amesema kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Man City ambacho timu yake imekipata katika Manchester Derby ni kati ya siku zake mbaya tangu awe kocha wa timu hiyo.
Man City ikiwa ugenini Old Trafford Jumapili hii iliibuka na ushindi huo mnono kwa mabao mawili ya Erling Haaland likiwamo moja na penalti pamoja na bao la tatu lililofungwa na Phil Foden.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Ten Hag aliulizwa na waandishi wa habari kama kipigo hicho kimeifanya siku iwe mbaya mno katika kazi yake, kocha huyo alijibu kwa kifupi, ‘ndio’.
“Ni kweli ni siku iliyonivuruga, mwaka jana tulikuwa na mengi mazuri, lakini unapopoteza mechi ya derby kwa namna ambavyo tumepoteza, hali hiyo inakuvuruga,” aliongeza Ten Hag.
“Nusu ya kwanza tulikuwa na mpango mzuri wa mechi na tuliifanyia kazi vizuri mipango yetu, kila kitu kilikuwa sawa, lakini baadaye penalti ikaharibu kila kitu na baada ya hapo kipindi cha pili tukaamua kuwa wenye kujilinda zaidi na mara ikawa 2-0 na kuanzia hapo mechi ikawa ngumu,” alisema Ten Hag.
Man United kwa matokeo hayo inazidi kujiweka pagumu, inashika nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu England (EPL) ikiwa nyuma wa vinara wa ligi hiyo, Tottenham kwa tofauti ya pointi 11.
Ten Hag hata hivyo alijifariji akisema kwamba anadhani timu yake ipo katika kuelekea kwenye mafanikio na kinachohitajika kwa sasa ni subira.
“Mechi tatu zilizopita tulishinda, na ari ilikuwa vizuri, nafikiri tunaelekea kwenye mafanikio, mwanzo ulikuwa mgumu lakini sasa tunaelekea pazuri, majeruhi wakianza kupona tutakuwa imara, tuwe na subira na nina furaha kwa sababu waliokuwa majeruhi wameanza kurudi na kikosi chetu kitakuwa imara,” alisema Ten Hag.
Matokeo ya mechi za Ligi Kuu England Jumapili…
West Ham 0-1 Everton
Aston Villa 3-1 Luton
Brighton 1-1 Fulham
Liverpool 3-0 Nottm Forest
Man Utd 0-3 Man City