Na mwandishi wetu
Mabao ya mastraika, Jean Baleke na Patrick Phiri yameiwezesha Simba kuwazamisha wababe wa Yanga, Ihefu FC kwa kutoka na ushindi wa 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu NBC.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Simba ndio waliokuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za Ihefu katika dakika ya 12 kwa bao la Jean Baleke.
Baleke alifunga bao hilo akitumia makosa ya beki wa Ihefu, Vedastus Mwihambi kukosa umakini baada ya kurudisha mpira nyuma na mfungaji kuunasa na kufumua shuti lililomshinda kipa Fikirini Bakari.
Ihefu chini ya kocha wao mpya Moses Basena walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika 12 baadaye kupitia kwa Ismael Mgunda aliyeuwahi mpira uliopigwa na Never Tigere na kuokolewa na kipa wa Simba, Ally Salim.
Kelele za mashabiki wa Simba kutaka kumuona mshambuliaji wao Phiri au Jenerali uwanjani zilisikiwa na kocha wao, Roberto Oliviera ya Robertinho ambaye alimpa nafasi na mchezaji huyo hakumuangusha. akaipatia Simba bao.
Phiri (pichani juu) ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Baleke, alifunga bao hilo dakika ya 65 akiitumia pasi ya Luis Miquissonne ambaye pia aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kibu Denis.
Ihefu katika mechi yake na Yanga msimu huu ilitoka na ushindi wa mabao 2-1 na kukawa na matumaini makubwa kwamba timu hiyo ingeweza kuizuia Simba.
Kwa ushindi huo Simba sasa imefikisha pointi 18 ikiwa na rekodi ya ushindi wa mechi ya sita mfululizo na inashika nafasi ya pili nyuma ya Yanga ambayo pia ina pointi 18 lakini imeshacheza mechi saba.
Soka Baleke, Phiri waizamisha Ihefu
Baleke, Phiri waizamisha Ihefu
Read also
