London, England
Eddie Nketiah kwa mara ya kwanza ameifungia Arsenal mabao matatu (hat trick) wakati timu hiyo ikiichapa Sheffield United 5-0 katika mechi ya Ligi Kuu England iliyochezwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Emirates.
Ushindi huo ambao umemfanya Nketiah aondoke uwanjani na mpira wa mechi hiyo pia umeipaisha Arsenal hadi nafasi ya pili katika ligi nyuma ya mahasimu wao wa London, Tottenham Hotspur ambao wanashika usukani.
Nketiah (pichani juu) ambaye alipata nafasi kikosi cha kwanza baada ya kuumia kwa Gabriel Jesus, aliitumia nafasi hiyo vizuri na kufungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 28 akiitumia vizuri pasi ya Declan Rice.
Katika mechi hiyo ambayo Arsenal iliitawala vyema, Nketiah alifunga mabao mengine katika dakika za 50 na 58 wakati mabao mengine yalifungwa na Fabio Vieira (kwa penalti) dakika ya 88 na Tomiyasu aliyefunga la tano katika dakika za nyongeza.
Nketiah angeweza kutoka uwanjani na mabao manne kama asingemuachia Vieira apige mkwaju wa penalti iliyotolewa baada ya Vieira kuchezewa rafu na Oliver Norwood.
Kama mchezaji huyo angepiga penalti na kufunga bao la nne angekuwa mchezaji wa tatu wa Arsenal kufunga idadi hiyo ya mabao kwenye mechi ya ligi, wengine ni Thierry Henry na Andrey Arshavin.
“Ni maajabu haikuwa rahisi, mwezi uliopita nilimpoteza shangazi yangu, kwa hiyo nataka niyatoe mabao haya matatu kama heshima kwake, familia yake ilikuwa hapa ikiangalia kwa hiyo hakika ni tukio la kipekee,” alisema Nketiah baada ya mechi hiyo.
Akizungumzia tukio la penalti hiyo, Nketiah alisema kwamba awali akili ilimtuma kuuchukua mpira huo ili apige penalti, “Fabio aliuwahi na lilikuwa tukio zuri, ni suala la mchezaji kwenye timu moja, ni kupata nafasi na kuitumia.”
Matokeo ya mechi za Ligi Kuu England leo Jumamosi…
Chelsea 0-2 Brentford
Arsenal 5-0 Sheff Utd
Bournemouth 2-1 Burnley
Wolves 2-2 Newcastle
