Na mwandishi wetu
Simba ya kibingwa imeaga kibingwa michuano mipya ya Ligi ya Soka Afrika (AFL) ikiangushwa na kanuni ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Al Ahly ya Misri katika mechi iliyopigwa Jumanne hii jioni.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita, Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 na vijogoo hao wa Afrika na ilihitaji ushindi wowote au sare ya zaidi ya mabao matatu ili kusonga hatua ya nusu fainali.
Simba licha ya kuwa ugenini mjini Cairo, Misri kwenye Uwanja wa Cairo, ilicheza soka la kujiamini kwa nidhamu ya hali ya juu ikiziba njia za Ahly na kufanya mashambulizi ya hapa na pale na haikushangaza timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana.
Matokeo hayo yaliibua matumaini makubwa kwa mashabiki wa Simba kwamba timu yao ilikuwa ikielekea kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayoshirikisha timu nane bora Afrika.
Nidhamu ya kiuchezaji na umakini wa kushambulia uliwafanya Simba wawe wa kwanza kuzitikisa nyavu za Ahly katika dakika ya 68 kwa bao lililofungwa kwa kichwa na Sadio Kanoute.
Kanoute alifunga bao hilo kwa mpira mrefu ulioanzia kwa Shomary Kapombe aliyepiga krosi ambayo iliunganishwa pia kwa kichwa na Jean Baleke kabla ya kumkuta mfungaji.
Bao hilo lilizidi kufufua matumaini ya Simba kuwabwaga vigogo hao wa soka la Afrika lakini mambo yaliharibika dakika nane baadaye, Ahly waliposawazisha bao hilo kupitia kwa Ally Maaloul ambaye aliitumia vizuri krosi ya Mahmoud Kahraba.
Simba kwa ujumla ilionekana kuwa na mpango mzuri katika mechi hiyo, haikuwa timu yenye woga wa kufanya mashambulizi na kutumia muda mwingi kujilinda badala yake ilicheza kwa utulivu, ikifunguka na bila kusahau kujilinda.
Mapema katika dakika ya 11 mipango hiyo ya Siimba ilionekana ilipofanya shambulizi lililoanzia kwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyefumua shuti ambalo hata hivyo lilitua mikononi mwa kipa wa Ahly, Mohamed El Shenawy.
Katika kipindi cha kwanza, Simba walijihami vizuri huku wakilisogelea mara kadhaa lango la Ahly wakimtumia zaidi mshambuliaji pekee John Bocco ambaye muda mwingi alicheza akiwa eneo la Ahly ambao pia walikuwa wakitibua vyema mipango ya Simba.
Kwa matokeo hayo, Simba inakuwa imeishia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ingawa italamba kitita cha Sh bilioni 2.5 ambazo zinapewa timu zilizofikia hatua ya robo fainali wakati zitakazofikia nusu fainali zitapewa Sh bilioni 4.3, nafasi ya pili Sh bilioni 7.5 na mshindi Sh bilioni 10.
Kimataifa Simba ya kibingwa yaaga AFL
Simba ya kibingwa yaaga AFL
1 Comment
Leave a Reply Cancel reply
Read also
asante sana kwa taarifa ila hii inaonesha kuwa mtandao wenu unaupendeleo sn hii habari leo siku ya tatu ndio inatoka punguzeni ushabiki ila hongerenei kwa kazi nzuri pia.