Na mwandishi wetu
Kung’oka kwa makocha wa klabu za Ligi Kuu NBC tangu kuanza msimu huu, kumewaibua baadhi ya makocha wazawa na kueleza kuwa vitendo hivyo havina afya na vinaweza kuzorotesha ukuaji wa timu.
Hiyo ni baada ya juzi kocha wa Namungo, Cedric Kaze kubwaga manyanga baada ya mechi sita na kabla yake Habibu Kondo aliyekuwa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila wa Ihefu na Hans Pluijm na Ernst Middendrop waliokuwa wakiinoa Singida Fountain Gate kwa nyakati tofauti kufungashiwa virago.
Kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Boniface Pawasa alisema: “Ni kama vile watu wanataka timu ijengwe siku moja au baada ya wiki kadhaa wakati ni suala la muda, haiwezekani kila mtu sasa hivi awe na uwezo wa kukosoa falsafa za makocha na kujiona anafahamu sana kuliko mwenye kazi yake.
“Kinachotokea kila mmoja kujiona mtaalamu wakati si kweli, tunawapa makocha presha ambazo hazina faida yoyote, tunawachanganya wachezaji kwa kuwabadilishia makocha kila wakati na hatujengi kwa mtindo huu, ni sawa na kujirudisha nyuma kwa kufukuza makocha kila baada ya mechi tano.”
Mchezaji huyo wa zamani wa Simba SC pia alimsifu Middendrop ambaye aliondoka baada ya kuisimamia Singida katika mchezo mmoja kwa kuwa aliingiliwa falsafa zake na viongozi na hakuwa tayari katika hilo kwa kuwa alifahamu wajibu na haki zake.
Naye beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ ameiambia GreenSports kuwa anaona taaluma ya makocha haiheshimiwi na baadhi ya wamiliki na viongozi wa timu kwa kuhisi wanafahamu zaidi kumbe wanaharibu mambo.
“Haiwezekani kocha afundishe kwa kipindi kifupi tu aondolewe, sasa timu inajengwa vipi? Viongozi wa mpira wanapaswa kuheshimu taaluma za makocha wa soka, angalau mtu anaweza kuulizwa baada ya mechi 10 ndipo unaweza kupata taswira lakini sio mechi tano au sita,” alisema Malima.
Kocha wa zamani wa Kagera Sugar, Mrage Kabange alisema kuwa viongozi wa timu wanapaswa kuelewa kuwa Ligi Kuu NBC imepanda chati duniani, imekuwa ngumu zaidi.
Aliwataka viongozi hao kuacha kutarajia mambo kuwa mepesi kama miaka ya nyuma na hawapaswi kuwa na mihemko ya kiushabiki kwani itadidimiza upya soka la nchi nzima.
