Na mwandishi wetu
Stephanie Aziz Ki kwa mara nyingine amedhihirisha thamani yake baada ya kufunga mabao matatu (hat trick) na kuiwezesha Yanga kupata ushindi wa 3-2 mbele ya Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu NBC.
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo Jumatatu jioni kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Aziz Ki alitumia vyema guu lake la kushoto kuipatia Yanga bao la kwanza dakika ya nane ya mchezo huo.
Azam ilijipanga na kusawazisha bao hilo dakika 10 baadaye mfungaji akiwa Djibril Silla ambaye kama Aziz Ki naye alitumia guu la kushoto kufunga bao hilo lililozifanya timu kwenda mapumziko zikiwa sare.
Mambo yaliwaharibikia Yanga katika dakika ya 61 walipofungwa bao la pili lililofungwa kwa penalti na Prince Dube baada ya Bakari Mwamnyeto kumchezea rafu Silla aliyekuwa akimkaribia kipa wa Yanga Djigui Diarra.
Penalti ya Dube iliingia upande wa kulia wa kipa Diarra ambaye aliuona mpira huo wa chinichini na kuufuata lakini shuti la Dube lilikuwa kali sana na kipa huyo kujikuta akiruka na kupishana na mpira.
Aziz Ki alizima matumaini ya Azam kutoka na ushindi dakika ya 68 ya mcheo huo kwa mara nyingine akipiga shuti la mguu wa kushoto lililomshinda kipa wa Azam, Idris Abdullah.
Kipa huyo kwa mara nyingine katika dakika ya 71 aliruhusu bao la tatu la Yanga baada ya kukosa umakini wakati akizuia shuti lingine la mguu wa kushoto la Aziz Ki kwa kuudaka mpira ambao ulimponyoka na kujaa wavuni.
Azam licha ya kupoteza mchezo huo lakini walionesha uhai na kulisumbua mara kwa mara lango la Yanga hasa katika dakika za majeruhi hali iliyowaweka mashabiki wa Yanga katika hofu.
Kwa upande mwingine mechi hiyo pia ilishuhudia burudani ya eneo la kiungo ambapo mara mbili, Feisal Salum au Fei Toto alimfanya mwamuzi Ahmed Arajiga awape kadi za njano Khalid Aucho na Mudathir Yahya.
Wakati Mudathir alipewa kadi hiyo kwa kumkaba kimabavu Fei Toto, Aucho yeye alipewa kadi hiyo kwa kumshika bukta Fei wakati akiwa tayari amemtoka.
Matokeo ya mechi ya leo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 15 katika ligi hiyo ikiwa nafasi ya kwanza baada ya kucheza mechi sita ikiwa na mabao 18 wakati Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 15 katika mechi tano na mabao 14 ya kufunga.
Azam inashika nafasi ya tatu na pointi zake 13 baada ya kucheza mechi sita ikiwa na mabao 12 ya kufunga.
Soka Aziz Ki apiga hat trick Yanga ikiiua Azam
Aziz Ki apiga hat trick Yanga ikiiua Azam
Read also
