Na mwandishi wetu
Kipa namba moja Singida Big Stars, Beno Kakolanya ameushukuru uongozi wa timu hiyo kwa kumpa tuzo ya mchezaji bora mwezi Septemba kwa timu hiyo lakini akieleza hilo lisingewezekana bila wachezaji wenzake.
Kakolanya (pichani juu) alipewa tuzo hiyo Jumatano hii chini ya udhamini wa Kampuni ya Jet & Sons, akiwa ni mchezaji wa kwanza kuchukua tuzo ya mwezi kwa timu hiyo tangu kuanzishwa kwake msimu huu.
“Nimefanikiwa kupata tuzo mwezi Septemba sijajua kwa miezi inayokuja maana hii ni kutokana na juhudi na mambo mengi uwanjani lakini hii yangu imetokana na ushirikiano wa wachezaji wenzangu uwanjani ndio msingi uliofanikisha haya,” alisema Kakolanya.
Kipa huyo ambaye alipewa tuzo hiyo na kitita cha Sh milioni moja amesema hiyo ni mara ya pili kupata tuzo hiyo kwani aliwahi kuinyakua wakati wa michuano ya Simba Super Cup iliyofanyika mwaka juzi ambapo pia alivuna zawadi ya Sh milioni moja.
Ofisa Habari wa Singida Big au Singida Fountain Gate, Hussein Masanza ameiambia GreenSports kuwa tuzo hiyo ya kwanza imetolewa kwa mujibu wa benchi la ufundi lakini tuzo zinazofuata utaandaliwa mchakato wa wazi.
Alifafanua kuwa katika mchakato huo wa wazi, mashabiki watashirikishwa kupendekeza mchezaji bora wa mwezi, akifafanua kuwa pia wameingia mkataba wa mwaka mmoja na Jet & Sons.
