Na mwandishi wetu
Siku chache baada ya kufutwa kazi na klabu ya Ihefu, kocha Zuberi Katwila (pichani) ameweka wazi kuwa hana muda wa kupumzika na anasikiliza ofa kutoka timu yoyote yenye maono mazuri ya kisoka.
Kocha huyo amezungumza hayo na GreenSports ikiwa takriban siku sita zimepita tangu aondolewe kuinoa Ihefu baada ya kuiongoza katika mechi tano pekee msimu huu akishinda mbili na kufungwa tatu.
“Siwezi kusema kwamba kuna timu fulani naisubiria au ni lazima nifundishe timu za ligi kuu peke yake, zipo timu nyingi zina mipango mizuri ya kisoka zipo madaraja ya chini, hivyo cha msingi ni sehemu yenye maono ya soka na ushindani nafikiri ndio nitaipa kipaumbele zaidi,” alisema Katwila.
Katwila aliyewahi kuinoa Mtibwa Sugar ya Morogoro alisema angeweza kupumzika kwa sasa lakini anahisi bado anahitaji kufanya vingi katika ukocha kwa sasa kuliko kupumzika kwa muda na kuwa nje ya mchezo.
“Naweza kupumzika lakini kwa sasa nahisi si muda sahihi sana wa kufanya hivyo sababu nina vitu vingi nahitaji kuvifanya kwenye soka na muda wa kupumzika ukifika nitapumzika kidogo kama kujipa likizo tu lakini kwa sasa bado kwanza,” alisema Katwila.
