London, England
Kiungo wa klabu ya Real Madrid, Jude Bellingham amesema anataka kuwa katika timu hiyo kwa miaka 10 akidai kwamba klabu hiyo imelifikisha soka lake katika kiwango kipya.
Bellingham alitoa mchango mkubwa katika ushindi wa mabao 3-1 ambao England uliupata katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Ulaya 2024 (Euro 24) iliyopigwa kwenye dimba la Wembley jana Jumanne.
Kwa msimu huu pekee, Bellingham ameshafunga jumla ya mabao 11 kwa timu ya England na klabu yake katika mechi 13 akiwa pia na asisti sita.
Bellingham aliyejiunga na Real Madrid akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya Euro milioni 103, alisema kwamba ameendelea kuwa bora kila wakati anapocheza.
“Ulikuwa usiku mzuri kwetu, sote tunakumbuka kilichotokea miaka michache iliyopita walipokuwa wakicheza nasi, wakati wote malengo huwa ni kupiga hatua, tunaelekea katika njia sahihi na huu ni ushindi muhimu kwetu,” alisema Bellingham.
“Nalipenda soka ninapokuwa nacheza, katika klabu na timu ya taifa napewa uhuru wa kucheza jinsi ninavyoona, tangu mwezi uliopita nimekuwa nikipigania kucheza niwe naingia kwenye ‘box’ na ninapofika nakuwa mwenye hasira,” alisema Bellingham.
Bellingham pia alisema kwamba baada ya uhamisho wake mkubwa wa kujiunga na Real Madrid ukweli ni kwamba kinachofuata ni matokeo katika uchezaji iwe ni kufunga magoli au kutoa asisti au kucheza katika kiwango cha kuipa timu ushindi,” alisema.
