Na mwandishi wetu
Baada ya kushindwa kupata ushindi kwenye michezo mitano ya Ligi Kuu NBC, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Mwinyi Zahera ameeleza kukerwa na matokeo hayo.
Coastal Union inaburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC wakiwa na pointi mbili baada ya mchezo mitano wakitoka sare mara mbili na kufungwa michezo mitatu.
Wagosi wa Kaya hao wamepoteza dhidi ya Azam FC bao 1-0, Simba mabao 3-0, kabla ya kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Dodoma Jiji huku ikiambulia suluhu mbele ya Tabora United na sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Zahera alisema kuwa kama mwalimu hafurahishwi kabisa na kipindi anachopitia hivi sasa baada ya kushindwa kupata ushindi wowote na sasa anarejea kujipanga kwa ajili ya michezo ijayo kuhakikisha anabadili mwelekeo.
“Hakuna mwalimu anayependa kuona anashindwa kupata matokeo katika michezo mfululizo hivyo nimeyaona mapungufu ya kikosi changu naenda kuyafanyia kazi makosa yote yaliyojitokeza katika michezo iliyopita ili turudi kwenye ubora wetu,” alisema Zahera .
Alisema kuwa huu ni wakati wa kushikamana pamoja na kuangalia madhaifu yao kitaalamu zaidi kabla ya kushuka uwanjani tena kuzisaka pointi tatu zitakazorudisha morali yao.
