Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga leo Jumatatu imesaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya shilingi milioni 900 na Kampuni ya Bima ya Taifa (NIC) kwa ajili ya kutoa tuzo za mchezaji bora wa mwezi.
Akizungumza katika hafla ya makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Rais wa Yanga, Hersi Said alisema mkataba huo utawapa wachezaji wa timu yake nafasi ya kutimiza majukumu yao uwanjani pamoja na kuendeleza mahusiano mazuri ya kibiashara na NIC.
Hersi alisema kimsingi makubaliano hayo yanakwenda kunufaisha pande zote husika kwani wakati Yanga ikinufaika kwa kupata shilingi milioni 900, NIC nao wanatapa fursa ya biashara yao kutangazwa kwa ukubwa.
“Wameamua kufanya kazi na sisi kwa sababu tuna wachezaji bora ambao huwezi kuwapata kwingine, ni wachezaji wenye ushawishi ndani na nje ya uwanja jambo ambalo ni chachu ya kutangaza biashara,” alisema Hersi.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa NIC, Elihuruma Doriye alisema kwamba historia nchini imeandikwa kwa taasisi mbili kuingia makubaliano ya kibiashara kwa kipindi cha miaka mitatu.
Doriye alisema kwamba kwa Tanzania huwezi kuzungumzia bima bila ya kuitaja NIC na kwa upande wa Yanga alisema kwamba klabu hiyo ni nembo ya soka la Tanzania.
“Ni furaha kubwa kupata fursa ya kufanya biashara na taasisi kubwa kama hii, kwa upande wetu NIC tumepewa hadhi ya kuaminika,” alisema Doriye.
Naye ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema klabu yao ina furaha kwa sababu mkataba huo utaongeza ushindani kwa wachezaji wa Yanga na hamasa itazidi kuwa juu kwa upande wa mashabiki.
Simba ilikuwa klabu pekee nchini iliyokuwa ikitoa tuzo za kila mwezi kwa wachezaji wake lakini tuzo hizo zilifutwa hivi karibuni baada ya aliyekuwa mdhamini. Kampuni ya Emirates Aluminium kumaliza mkataba na klabu hiyo.
