Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumamosi imenyakua pointi tatu muhimu baada ya kuichapa Geita Gold mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba mjini Mwanza.
Bao la kwanza la Yanga lilipatikana dakika moja kabla ya timu hizo kwenda mapumziko mfungaji akiwa ni Pacome Zouazoua akiitumia pasi ya beki Yao Kouasi.
Dakika moja baadaye, Geita walishangazwa kwa kuchapwa bao la pili lililofungwa na Stephanie Aziz Ki ambaye aliinasa krosi ya Maxi Nzengeli na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili Yanga waliendelea kuisakama Geita na hatimaye kuandika bao la tatu lililofungwa na Maxi katika dakika ya 67.
Kwa ushindi huo Yanga sasa imefikisha pointi 12 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Azam ingawa huenda ikashuka zaidi kutegemea matokeo ya mechi ya Jumapili ya Simba dhidi ya Singida Fountain Gate. Simba pia ina pointi 12.
Katika mechi hiyo, Geita ilijikuta katika wakati mgumu mapema dakika ya 14 baada ya mshambuliaji wake tegemeo na nahodha wa timu hiyo, Elius Maguli kuumia wakati akiwania mpira wa juu na beki wa Yanga, Bakari Mwamnyeto.
Mechi ya leo pia iliathiriwa na mvua ambayo ilinyesha muda mfupi kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza kwa takriban dakika tatu kabla ya kukatika.
Soka Yanga yaipopoa Geita 3-0
Yanga yaipopoa Geita 3-0
Read also
