Na mwandishi wetu
Timu ya JKT Tanzania imeanza haraka marekebisho ya uwanja wake wa CCM Kambarage, ikisema inapambana kuhakikisha unafunguliwa kabla ya mchezo wao wa nyumbani unaofuata.
Akizungumza na GreenSports, Ofisa Habari wa JKT, Masau Bwire (pichani) alisema kwamba walianza zoezi la kuirekebisha Kambarage mapema baada ya juzi kupokea barua kutoka Bodi ya Ligi ya kufungwa kwa uwanja huo kwa kutokidhi vigezo.
“Tunapambana kuona namna ya kushughulikia haya mapungufu. Tumeshaanza kwa nguvu kubwa kufanya marekebisho tukiamini mpaka kufikia siku ya mchezo wa nyumbani Oktoba 28 dhidi ya Tabora United tutakuwa tayari,” alisema Bwire.
Bwire alisema wanafahamu kikanuni uwanja unakaguliwa na kupitishwa siku saba kabla ya mechi, hivyo wanapambana kuhakikisha unakamilika mapema na kuja kufanyiwa ukaguzi na kuthibitishwa uwanja wao huo kabla ya Oktoba 21.
Uwanja wa Kambarage ulifungiwa na Bodi ya Ligi baada ya mchezo wao wa hivi karibuni dhidi ya Mashujaa ambao JKT walishinda kwa bao 1-0.
Uwanja huo ulifungiwa kwa madai ya kutokuwa tambarare na kukosa nyasi eneo la kuchezea, ukikosa vigezo vya kanuni na sheria za mpira wa miguu.
Soka JKT waanza marekebisho CCM Kambarage
JKT waanza marekebisho CCM Kambarage
Read also
