Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Hemed Seleman ‘Morocco’ ameahidi kuifunga Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu NBC utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Morocco alisema imani hiyo inatokana na maandalizi wanayoyafanya pamoja na mapungufu aliyoyabaini kwa wapinzani wao hao kupitia mchezo wa majuzi waliofungwa na Ihefu mabao 2-1.
“Tutatumia mbinu za Ihefu kuifunga Yanga, najua hautokuwa mchezo rahisi sababu hawatotaka kupoteza mechi mbili mfululizo lakini tumewaandalia huzuni nyingine Jumamosi,” alisema Morocco.
Kocha huyo alisema lengo lao ni kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi wakiwa katika nafasi nne za juu na kampeni hiyo itaanzia kwenye mchezo huo dhidi ya mabingwa hao watetezi, akiamini ushindi dhidi ya Yanga utaamsha zaidi morali yao ya mapambano.
Geita kwa sasa inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi nne katika idadi kama hiyo ya mechi ilizocheza tangu kuanza msimu huu.
