Isfahan, Iran
Mechi ya Ligi ya Mabingwa Asia kati ya timu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia na Sepahan ya Iran imeshindwa kuchezwa baada ya Al Ittihad kugoma wakipinga uwapo wa sanamu ya Jenerali Qasem Soleimani wa Iran iliyopo sehemu ya kuingilia uwanjani.
Al-Ittihad inayonolewa na kocha wa zamani wa timu za Tottenham na Wolves, Nuno Santo ikiwa na wachezaji mastaa waliotamba Ulaya kina N’Golo Kante na Fabinho sanamu ya jenerali huyo aliyeuawa.
Kutochezwa kwa mechi hiyo iliyokuwa ichezwe Jumatatu jioni, kumewakwaza mashabiki wapatao 60,000 waliofika kwenye Uwanja wa Naghsh mjini Isfahan kwa ajili ya mechi hiyo.
Saudi Arabia na Iran zimekuwa na mgogoro wa kisiasa kwa muda mrefu sasa hali iliyosababisha mechi zinazohusisha klabu za nchi hizo mbili kuchezwa katika viwanja huru tangu mwaka 2016 kutokana na hofu ya kiusalama.
Shirikisho la Soka Asia (AFC) katika taarifa yake iliyotolewa baadaye ilieleza kuwa mechi hiyo imefutwa kwa lengo la kuchukua tahadhari ya hofu juu ya uwezekano wa kutokea vurugu na matukio mengine.
“AFC inasisitiza kujitoa kwake katika kuhakikisha usalama na amani kwa wachezaji, maofisa wa mechi, watazamaji na wadau wengine wanaohusika, kilichotokea kitajadiliwa katika kamati husika,” ilifafanua taarifa ya AFC.
Jenerali Qasem Soleimani aliuawa na majeshi ya Marekani mwaka 2020 na ingawa amekuwa akionekana kuwa shujaa nchini Iran, lakini tangu mwaka 2018 Saudi Arabia imekuwa ikimhusisha jenerali huyo na baadhi ya makamanda wake katika matukio ya kigaidi.
