Manchester, England
Majanga yameendelea kuiandama Man United msimu huu baada ya jana Jumanne kufungwa mabao 3-2 na Galatasaray katika Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikimaliza mechi hiyo na wachezaji 10.
Katika mechi hiyo, Man United ilishindwa kulinda mabao iliyoyapata na kujikuta ikishindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani na huo kuwa mwendelezo usiofaa wa klabu hiyo msimu huu.
Man United ilipata bao la kwanza dakika ya 17 lililofungwa na Rasmus Hojlund lakini Galatasaray walisawazisha kupitia kwa nyota wa zamani wa Man United, Wilfred Zaha.
Hojlund, mshambuliaji mpya wa Man United kwa mara nyingine aliifungia timu hiyo bao la pili dakika ya 67 lakini kwa mara nyingine Galatasaray walisawazisha dakika nne baadaye kupitia kwa Kerem Akturkoglu.
Dakika sita baada ya kuingia bao hilo, Man United walipata janga baada ya kiungo Casemiro kupewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Dries Mertens ambaye alikuwa akielekea kumtungua kipa Andre Onana wa Man United.
Rafu hiyo ya Casemiro ilizaa penalti ambayo Mauro Icardi alishindwa kuitumia kuipa Galatasary bao ingawa ni Icardi huyo huyo aliyefuta kosa hilo kwa kuifungia timu yake bao la tatu katika dakika ya 81.
Matokeo hayo yanazidi kumuweka pagumu kocha Erik ten Hag ambaye timu yake inashika mkia katika kundi lake ikiwa nyuma kwa tofauti ya pointi nne na vinara wa kundi hilo Bayern Munich.
Hiki ni kipigo cha pili mfululizo kwa Man United baada ya kushindwa kutamba mbele ya Crystal Palace katika Ligi Kuu England mwishoni mwa wiki na ni kipigo cha tano katika mechi saba zilizopita.
“Mwanzo wetu wa msimu haujawa mzuri, ingawa zipo sababu hatuwezi kujaribu kujificha kwa vijisababu, ni juu yetu kubadili mambo, kitakachotokea hapo baadaye ni juu yetu na si mwingine yeyote,” alisema Ten Hag.
Matokeo ya mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya za jana Jumanne
Union Berlin 2-3 Sporting Braga
Man Utd 2-3 Galatasaray
Lens 2-1 Arsenal
Napoli 2-3 Real Madrid
RB Salzburg 0-2 Real Sociedad
FC Copenhagen 1-2 Bayern Munich
PSV Eindhoven 2-2 Sevilla
Inter Milan 1-0 Benfica