London, England
Kocha wa Tottenham Hotspur, Ange Postecoglou (pichani) amesema hapendi matumizi ya VAR kwa kuwa yanasababisha utata licha ya timu yake kunufaika na makosa ya mfumo huo katika mechi yao na Liverpool Jumamosi.
Jopo la waamuzi walikiri kwamba yalifanyika makosa kukataa bao la Liverpool lililofungwa na winga, Luis Díaz kipindi cha kwanza na mwishowe ni Spurs iliyokuwa nyumbani ambayo ilitoka na ushindi wa mabao 2-1.
“Nafikiri nipo kwenye rekodi kwa kauli yangu ya kwamba sikuwahi kuwa shabiki wa VAR tangu kuanza kwake kutumika,” alisema Postecoglou, kocha wa zamani wa Celtic.
“Si kwa sababu nyingine yoyote zaidi ya fikra kwamba inasababisha utata katika baadhi ya maeneo ya mchezo ambayo nilidhani yalikuwa wazi siku za nyuma lakini naweza kuona kwamba ni teknolojia ambayo ingekuja tu, ni lazima tukabiliane nayo,” alisema Postecoglou mbele ya waandishi wa habari.
“Mchezo wa soka una historia ya kugubikwa na maamuzi ya waamuzi ambayo hayawi sahihi lakini sote tuliyakubali kama sehemu ya mchezo kwa sababu tunafanya kazi na binadamu,” alisema Postecoglou.
“Nafikiri watu walikuwa na fikra zisizo sahihi kwamba VAR haitokuwa na makosa, sidhani kama kuna teknolojia ya hivyo kwa sababu mambo mengi katika mchezo wetu hayako sahihi, ni suala la tafsiri na yote yanafanywa kwa uwezo wa binadamu,” alisema Postecoglou.
Katika mechi hiyo Joel Matip wa Liverpool alijifunga katika dakika za lala salama wakati timu yake ikiwa na wachezaji tisa uwanjani baada ya kutolewa kwa kiungo Curtis Jones na winga Diogo Jota.
Akizungumzia matokeo hayo, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alisema kwamba uamuzi wa VAR kuwanyima bao ulibadili kwa kiasi kikubwa mwelekeo na kasi ya mchezo.