Na mwandishi wetu
Yanga imeeleza kuwa na maandalizi ya kutosha kwa mechi yao ya kesho Jumamosi dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan ili kupata matokeo chanya na kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameeleza hayo leo Ijumaa kwamba licha ya kufahamu kuwa Yanga ina kiu ya kufika makundi lakini yeye binafsi anahitaji kulifanikisha hilo kwa kuwa ni miongoni mwa yaliyomleta kuinoa timu hiyo.
“Tuna dakika 90 za kupambania tunachotaka kukipata, kufuzu makundi. Maandalizi yalikuwa mazuri na tulipata muda mwingi wa kujiandaa, tumefanya maandalizi makubwa kuhakikisha kesho tunacheza mechi nzuri na kuwapa furaha familia ya Wananchi.
“Kila kitu kipo sawa na nitaweka kikosi cha kwanza ambacho kitakuwa na mbinu tofauti na kwenye mechi ya ugenini, tutarekebisha makosa ya mechi ya kwanza ili tupate ushindi maana tutaingia uwanjani kama vile matokeo ni 0-0,” alisema Gamondi.
Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Pele, Kigali, Rwanda wiki mbili zilizopita.
Na kwenye mechi ya kesho itakayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 1.00 jioni, Yanga inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote kutinga makundi.
Kocha wa Al-Merreikh, Osama Nabieh alisema: “Japokuwa Yanga ni timu ngumu kwa sasa lakini tumekuja hapa kutafuta matokeo na lolote linawezekana kama wao walipotufunga mechi ya kwanza.
“Dakika 90 za kesho zitajibu maswali yote, si kitu rahisi kufunga bao kwenye soka, tuliruhusu mabao mawili sababu tulifanya makosa ambayo kwenye soka yapo na tutayatumia pia makosa ya Yanga kwa ajili ya kufanikisha malengo yetu.”
