Na mwandishi wetu
Jean Baleke ameuwasha moto Ligi Kuu NBC baada ya kufunga mabao matatu (hat trick) yaliyoipa Simba ushindi wa 3-0 dhidi ya Coastal Union katika mechi iliyopigwa Alhamisi hii kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mabao hayo yanamfanya Baleke kushika usukani kwenye orodha ya wafungaji wa ligi hiyo akiwa na mabao matano na kumpiku Fei Toto wa Azam FC anayeshika nafasi ya pili akiwa na mabao matatu.
Kwa mabao hayo, Beleke pia anakuwa amefufua matumaini mapya kwa mashabiki wa Simba baada ya kujikuta katika wakati mgumu kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Power Dynamos ya Zambia iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Ndola, Zambia mwishoni mwa wiki iliyopita, mshambuliaji huyo kutoka DR Congo alishindwa kuzitumia nafasi nyingi za wazi ambazo zingeweza kuifanya timu hiyo itoke na ushindi wa ugenini.
Baleke hata hivyo alikuwa tofauti katika mechi na Coastal akianza kuzichana nyavu za wapinzani wao katika daika ya saba ya mchezo alipomalizia vizuri pasi ya Mwamba wa Lusaka, Clatous Chota Chama.
Kwa mara nyingine Baleke akawainia tena vitini mashabiki wa Simba dakika nne baadaye safari hii akiitumia vizuri pasi ya beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Karamu ya mabao ya Simba ilihitimishwa na Baleke dakika tano kabla ya timu kwenda mapumziko akifunga kwa mkwaju wa penalti baada ya Luis Miquisson kufanyiwa madhambi.
Coastal inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera, ikimtumia nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Azam, Ibrahim Ajibu ilijitahidi kupeleka mashambulizi ya hapa na pale kwenye lango la Simba lakini juhudi za timu hiyo hazikuweza kuzaa matunda hadi dakika 90 za mchezo zinakamilika.
Katika mechi hiyo, Coastal ilipata pigo mapema dakika ya 21 baada ya Hija Ugando kupewa kadi nyekundu na mwamuzi Ahmed Arajiga kwa kumchezea rafu Henock Inonga wa Simba wakati wakiwania mpira.
Tukio hilo licha ya kuifanya Coastal icheze pungufu lakini pia limeibua hofu katika kikosi cha Simba kwani Inonga baada ya rafu hiyo alilazimika kutoka na kupelekwa hospitali kwa gari la wagonjwa huku wachezaji hasa wa Simba wakionekana wenye huzuni.
Inonga alikuwa ndio kwanza ametoka kupona majeraha ya bega aliyoyapata katika mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Yanga, mechi ambayo Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti.
Kocha wa Simba, Roberto Olivieira, Robertinho’ kwa mara nyingine alimpa nafasi kipa Ayoub Larked ambaye alikuwa akilalamikiwa kwa kucheza chini ya kiwango mechi na Power Dynamos hasa kwa kufungwa kizembe bao la pili lakini washambuliaji wa Coastal hawakuweza kumtungua.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyopigwa baadaye usiku, Singida Fountain Gate ilishindwa kutamba mbele ya Azam ilipolala kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complexa, Chamazi, Dar es Salaam.
Soka Moto wa Baleke Ligi Kuu NBC
Moto wa Baleke Ligi Kuu NBC
Read also