Na mwandishi wetu
Licha ya uwepo wa uvumi wa kuondoka kambini kwa Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Ernst Middendorp (pichani) ikielezwa amehitilafiana na klabu hiyo, uongozi wa klabu umekanusha taarifa hizo.
Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza amekiri kuondoka kwa kocha huyo lakini akaeleza hakuna mgogoro wowote baina yao zaidi ya kocha kuamua kwenda kuweka mambo yake binafsi sawa kabla ya kurejea kazini.
“Ni kweli kocha wetu Ernst amepata dharura na ameondoka kwa dharura lakini si kwa sababu zinazotajwa, ifahamike kocha naye ni binadamu, kuna changamoto zake binafsi anapitia na ameenda kuzitatua.
“Nafikiri kwa sasa tumpe nafasi na tumuombee azimalize mapema ili arejee kwenye majukumu yake maana bado hatujamaliza kibarua chetu na Mwarabu (Future FC),” alisema Masanza.
Kuondoka kwa kocha huyo kumekuja siku chache tangu timu hiyo iibuke na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Future FC ya Misri kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Na miongoni mwa sababu zilizotajwa katika mgogoro huo ni upangaji wa kikosi chake kilichovaana na Future, ikielezwa uongozi haukufurahishwa na hilo.
Kwa sasa timu hiyo ipo chini ya kocha msaidizi, Mathias Lule ikiendelea na maandalizi ya mechi yao dhidi ya Azam FC itakayopigwa keshokutwa Alhamisi kwenye, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Soka Singida yataja sababu za kocha kuondoka
Singida yataja sababu za kocha kuondoka
Read also
