Na mwandishi wetu
Beki wa kati wa Azam FC, Abdallah Kheri ‘Sebo’ analazimika kukaa nje ya uwanja kwa miezi mitatu baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti lake la mguu wa kulia.
Sebo amefanyiwa matibabu hayo kwenye hospitali ya Vincent Palloti, Cape Town, Afrika Kusini baada ya kupata majeraha kwenye mechi ya ligi iliyopita dhidi ya Prisons waliposhinda kwa mabao 3-1.
Daktari wa Azam, Mwanandi Mwankemwa aliyeambatana na beki huyo alisema Sebo amefanyiwa upasuaji wa gegedu ya maungio ya goti ambayo imeumiza mifupa midogo midogo kutokana na mlalo wa goti hilo.
“Sebo amefanyiwa upasuaji wa kisasa unaoitwa ‘arthroscopic’, ambao wametoa mifupa midogo midogo iliyokuwa imevunjika na kupandikiza gegedu nyingine,” alisema Mwankemwa akimzungumzia mchezaji huyo aliyefanyiwa upasuaji Jumatatu hii.
“Sasa baada ya kufanyiwa upasuaji huo, mchezaji huyo ameelekezwa mazoezi ya kufanya kwa muda wa mwezi mzima na anatakiwa kupumzika kwa muda wa miezi mitatu,” alisema Mwankemwa.