Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amemkingia kifua kipa mpya wa timu hiyo, Ayoub Lakred akisema hastahili lawama kwa kilichotokea Jumamosi kwenye mchezo wao dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.
Kipa huyo alidaka mechi yake ya kwanza Jumamosi na kufungwa mabao mawili ambayo mashabiki wa timu hiyo wanadai kuwa ni mepesi ukilinganisha na ukubwa wa timu hiyo.
Akizungumza na Mtandao wa Simba, Robertinho alisema kipa huyo raia wa Morocco hastahili lawama kwani alikuwa na mchango mkubwa katika mechi hiyo na alipaswa apongezwe kwa kuwa ndio ulikuwa mchezo wake wa kwanza tangu ajiunge na Simba.
“Lakred ni kipa mwenye kipaji ndio maana amejiunga na timu kubwa kama Simba, yawezekana alifanya makosa, ni kitu cha kawaida kwenye mchezo wa soka lakini hastahili kubebeshwa lawama sababu hakucheza peke yake,” alisema Robertinho.
Kocha huyo alisema mipango yake ni kuendelea kumpa nafasi Lakred aliyetua msimu huu akitokea FAR Rabat ya Morocco katika mechi zijazo ikiwemo za Ligi Kuu NBC, na anaamini ataisaidia timu hiyo ifikie malengo ambayo wamejipangia msimu huu.
Katika mchezo huo wa kwanza kwa Lakred, Simba ilipata matokeo ya sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
