Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe ameuanza vizuri msimu mpya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufunga bao wakati timu yake ikiilaza Borussia Dortmund mabao 2-0 na kuibua matumaini mapya.
PSG katika miaka ya karibuni ikiwa na wachezaji mastaa Lionel Messi, Neymar na wengineo imekuwa ikishindwa kufurukuta katika michuano hiyo na badala yake kuishia kutamba katika Ligi 1 ya Ufaransa.
Messi na Neymar wameihama timu hiyo, Messi akitimkia nchini Marekani katika klabu ya Inter Miami wakati Neymar amejiunga na Al Hilal ya Saudi Arabia.
Katika mechi na Dortmund iliyopigwa jana, Mbappe alifunga bao kwa mkwaju wa penalti dakika ya 49 baada ya Nicklas Sule kuunawa mpira uliopigwa na mshambuliaji huyo na mwamuzi kuamuru ipigwe penalti.
Bao la pili la PSG lilipatikana katika dakika ya 58 mfungaji akiwa ni beki Achraf Hakimi baada ya kushirikiana vizuri na kiungo Vitinha aliyemuunganishia pasi ya kisigino.
PSG waliutawala vyema mchezo huo tangu mwanzo lakini juhudi zao zilikatishwa tamaa na Dortmund hususan katika kipindi cha kwanza.
Ushindi huo unakuwa wa kwanza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kocha mpya wa timu hiyo Luis Enrique ambaye pamoja na mambo mengine ana jukumu zito la kuipa mafanikio hasa kwenye ligi hiyo ya klabu barani Ulaya ambayo ni kubwa na maarufu duniani kote.
Matokeo ya mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya za jana Jumanne ni kama ifuatavyo…
AC Milan 0-0 Newcastle
Feyenoord 2-0 Celtic
Lazio 1-1 Atl Madrid
PSG 2-0 B Dortmund
Man City 3-1 Red Star Belgrade
Barcelona 5-0 Royal Antwerp
Young Boys 1-3 RB Leipzig
Shakhtar Donetsk 1-3 FC Porto
Kimataifa Mbappe aibeba PSG Ligi ya Mabingwa
Mbappe aibeba PSG Ligi ya Mabingwa
Read also
