Madrid, Hispania
Polisi nchini Hispania wamewakamata wachezaji watatu wa timu ya vijana ya Real Madrid wakidaiwa kusambaza video inayodaiwa kuwa na maudhui ya ngono ikiwahusisha watoto wa umri mdogo.
Tukio hilo limetokea wakati huu habari kubwa Hispania ikiwa ni kashfa ya aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania, Luis Rubiales aliyelazimika kujiuzulu baada ya kumbusu mdomoni mshambuliaji wa timu ya wanawake, Jenni Hermoso.
Wachezaji hao ambao umri wao si mdogo baadaye waliachiwa kwa maagizo ya mahakama baada ya polisi kuhifadhi matukio yote yaliyorekodiwa kwenye simu zao kupitia WhatsApp.
Mapema Alhamisi hii, uongozi wa klabu ya Real Madrid ulithibitisha mmoja wa wachezaji wao katika kikosi cha akiba maarufu Castilla kukamatwa pamoja na wachezaji wengine watatu wa timu C kuhojiwa na taarifa zao kurekodiwa polisi wakihusishwa na usambazaji wa video binafsi kupitia mtandao wa WhatsApp.
“Mara baada ya klabu kupata taarifa za tukio zima, itachukua hatua stahiki,” ilieleza kwa kifupi taarifa ya klabu ya Real Madrid.
Polisi walithibitisha kuwa wachezaji watatu wamekamatwa na kuwekwa katika eneo la uwanja wa michezo wa klabu ya Real Madrid wakati mchezaji wa nne akiendelea kuhojiwa.
Kukamatwa na kuhojiwa kwa wachezaji hao kulitokana na hatua ya mwanamke mmoja mwenye mtoto wa kike wa miaka 16 kuwasilisha malalamiko polisi kuhusu kurekodiwa video yenye maudhui ya ngono.
Polisi walidai kuwa msichana huyo alikiri kuwa na urafiki na mhusika lakini tukio la kurekodi video hiyo lilifanyika mwezi Juni bila ya ridhaa yake na aligundua hilo hivi karibuni.
