Na mwandishi wetu
Benchi la ufundi la timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars limeeleza kuwa tayari limeshaanza maandalizi kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) inayotarajia kuanza kuunguruma Januari, mwakani nchini Ivory Coast.
Kocha Msaidizi wa Stars, Hemed Morocco ameiambia GreenSports leo Jumatano kuwa walishaanza kujipanga kuhusiana na michuano hiyo siku moja baada ya kufuzu kutokana na matokeo ya suluhu dhidi ya Algeria na hivyo kumaliza nafasi ya pili Kundi F ikiwa na pointi nane dhidi ya Uganda yenye saba na Niger yenye mbili.
Alisema wao kama benchi wameanza mikakati wakiwa na dhamira ya kukisuka kikosi cha ushindani pamoja na program sahihi za kuhakikisha wanakwenda kufanya vizuri katika michuano hiyo.
“Baada ya kupata nafasi tu, tulikaa na kujadili cha kufanya, tumejua tuna kazi ya kufanya na tumeanza maandalizi tayari, tunaangalia program za kufanya katika maandalizi ingawa mipango yetu inasubiri muunganiko wa taasisi nyingine ili tujue tunaanza vipi au tuna changamoto ipi,” alisema Morocco.
Pia kocha huyo alifafanua kuwa wamebaini yapo mengi ya kurekebisha ndani ya kikosi ili angalau kupata kitu bora ambacho kiatwafurahisha Watanzania kwa ujumla.
Alieleza kuwa wanahitaji sapoti ya Watanzania wote kuelekea michuano hiyo ndio maana wanasuka mipango madhubuti na kuhakikisha wanafanya vizuri kuliko michuano mingine iliyopita waliyowahi kushiriki.
Hii ni mara ya tatu, Tanzania inashiriki michuano hiyo ya makala ya 34 sasa ambayo bingwa mtetezi ni Senegal baada ya kushiriki mwaka 1980 nchini Nigeria kisha mwaka 2019 nchini Misri na kuishia hatua ya makundi.
