Madrid, Hispania
Rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF), Luis Rubiales (pichani) hatimaye amejiuzulu nafasi yake baada ya kuandamwa na tukio la kumbusu mdomoni mshambuliaji wa timu ya wanawake ya Hispania, Jenni Hermoso.
Rubiales aliyembusu Jenni Agosti 20 baada ya Hispania kuibwaga England bao 1-0 na kubeba taji la dunia, awali alitangaza kutokuwa tayari kujiuzulu akisisitiza hajafanya jambo lolote baya, aliwasilisha barua ya kujiuzulu Jumatatu hii kwa rais wa muda wa REEF, Pedro Rocha.
Mbali na kujiuzulu REEF, Rubiales pia ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya makamu rais wa Umoja vya Vyama vya Soka Ulaya (Uefa)
Kujiuzulu kwa Rubiales huenda kukapunguza shutuma zilizokuwa zikielekezwa kwake kutoka makundi mbalimbali yaliyomtaka ajiuzulu wakiwamo wachezaji wa timu ya wanawake Hispania waliotangaza kutoichezea timu hiyo kama Rubiales angeendelea kukalia kiti cha REEF.
Wakati Rubiales akichukua uamuzi wa kujiuzulu, Jenni, 33, ameshalifikisha suala hilo kwenye vyombo vya sheria akisisitiza kwamba hakukuwa na makubaliano ya yeye kupigwa busu mdomoni.

Katika madai yake ya awali, Rubiales, 46, alisisitiza kwamba hawezi kujiuzulu na kwamba kulikuwa na makubaliano baina yake na Jenni ingawa Fifa walimsimamisha kwa siku 90 na kutangaza kuanza uchunguzi wa tukio hilo.
“Baada ya kusimamishwa haraka kulikofanywa na Fifa pamoja na kufunguliwa mashtaka dhidi yangu, ni dhahiri kwamba siwezi kurudi katika nafasi yangu,” alisema Rubiales.
“Kusisitiza kusubiri na kushikilia msimamo hakutachangia jambo lolote chanya kwa shirikisho la soka Hispania au soka la Hispania,” alisema Rubiales kuutetea uamuzi wake wa kujiuzulu.
“Nina imani katika ukweli na nitafanya kila liwezekanalo kwa uwezo wangu ukweli uwekwe wazi,” alisema Rubiales.
“Wanangu (wa kike) watu wa familia yangu na watu wanaonipenda wameumizwa na matokeo ya adhabu ninayopewa pamoja na kuwapo kwa uwongo mwingi lakini pia upo ukweli kwamba mitaani siku hadi siku ukweli umeendelea kujiweka wazi,” alisema Rubiales.
“Baba yangu, wanangu, hao nimezungumza nao, wanajua hapa si tena suala langu, na baadhi ya marafiki wa karibu wameniambia, Luis ni lazima uangalie hadhi yako na kuendelea na maisha yako kwa sababu tofauti na hivyo utawaumiza watu unaowapenda na mchezo unaoupenda,” alisema Rubiales.
“Hili si suala langu peke yangu, misimamo yangu inaweza kuwaumiza watu wengine ambao ni muhimu, ni jambo la busara kwa uamuzi niliouchukua,” alisema Rubiales.
