Na mwandishi wetu
Historia mpya, timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefuzu kushiriki fainali za soka za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2024 baada ya sare ya 0-0 na wenyeji Algeria, Alhamisi hii usiku kwenye Uwanja wa Mei 19 mjini Anaba, Algeria.
Hii inakuwa mara ya tatu kwa Stars kufuzu kushiriki fainali hizo, ikiwa imeshiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1980 na baada ya hapo ikashiriki kwa mara nyingine mwaka 2020 nchini Misri na sasa inasubiri kushiriki mara ya tatu mwaka 2024 nchini Ivory Coast.
Stars iliyokuwa Kundi F imefuzu ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Algeria ambayo tayari ilikuwa imefuzu ikiwa na pointi 16 wakati Stars imefikisha pointi nane na Uganda Cranes imeishia nafasi ya tatu na pointi zake saba.
Algeria ikimtumia nyota wa zamani wa Man City, Riyad Mahrez ambaye kwa sasa anaichezea, Al-Ahli ya Saudi Arabia, ilianza mechi na Stars kwa kujiamini ikicheza pasi fupi na katika dakika ya kwanza ya mchezo huo ililishambulia lango la Stars na kuwapa wakati mgumu mabeki.
Dakika ya nne, krosi ya Badredine Boanani aliyemtoka Novatus Dismas ilizua kizazaa langoni mwa Stars lakini mpira uliopigwa na Kadri ulitoka nje ya lango.
Stars walianza kujibu mapigo dakika ya nane kwa kupata kona mbili zilizotokana na juhudi za Mzamiru Yassin lakini kona zote hizo zilizopigwa na Haji Mnoga ziliokolewa na mabeki wa Algeria.
Stars ilitumia muda mrefu wa kipindi cha kwanza kulinda lango lao hali iliyowapa nafasi Algeria kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara na dakika chache kabla ya mapumziko timu hiyo ilipoteza nafasi mbili za kupata mabao.
Katika mechi hiyo, Stars ilifanya mabadiliko kadhaa kwa kumtoa Clement Mzize na kumuingiza Abdul Sopu ambaye baadaye aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Himid Mao ambaye ni kama vile aliingia kuimarisha eneo la ulinzi.
Wakati muda wa mchezo kumalizika ukikaribia, mashabiki wa Algeria walionekana kukata tamaa na kuchukizwa na matokeo hayo ambayo yamepokelewa kwa shangwe na vigelegele na mashabiki wa soka nchini Tanzania ambao waliishuhudia mechi hiyo usiku huu kupitia televisheni katika maeneo mbalimbali ikiwamo majumbani na kwenye klabu za starehe.
Uganda Cranes iliyokuwa ikiumana na Niger iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ambao haukutosha kuzima ndoto za Stars kuweka rekodi ya kufuzu fainali za Afcon kwa mara ya tatu. Maombi ya Uganda ilikuwa ni kwa Stars kupoteza mechi na Algeria jambo ambalo halikufanikiwa.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2019 Stars ilihitaji kuifunga Uganda Cranes ili ifuzu fainali za 2020 jambo ambalo ililifanikisha kwa kuichapa timu hiyo mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kama ilivyokuwa kwa Algeria safari hii ambayo ilicheza mechi na Stars ikiwa imefuzu fainali za 2024, Uganda Cranes nayo mwaka 2019 ilicheza mechi ya mwisho na Stars ikiwa imefuzu fainali za 2020.
Kabla ya mechi ya Stars na Uganda ya mwaka 2019, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanaifunga Stars licha ya kuwa tayari wamefuzu lakini mwishowe ni Stars waliotoka uwanjani na ushindi.
Kimataifa Stars yafuzu Afcon mara ya tatu
Stars yafuzu Afcon mara ya tatu
Read also