Na mwandishi wetu
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) leo Alhamisi wamezindua rasmi chapa mpya ya Ligi ya NBC Championship pamoja na uzinduzi wa michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Septemba 9, mwaka huu.
Hiyo ni kutokana na udhamini wa NBC walioingia hivi karibuni wa michuano hiyo sambamba na mwendelezo wa udhamini wa ligi kuu wenye thamani ya Sh bilioni 32 mpaka mwaka 2027.
Akizungumza Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Binafsi wa NBC, Elibariki Masuke alisema huo ni mwendelezo wa mkakati wa benki hiyo kuiboresha zaidi ligi hiyo kwa kuangazia misingi muhimu ikiwemo kukuza vipaji vya wachezaji na kuongeza ushindani kwenye mchezo huo.
“Ni wazi kwa sasa soka hususani ligi yetu imegeuka kuwa si tu kivutio kwa mamilioni ya wapenda mchezo huu bali pia ni jukwaa wezeshi la kijamii na kiuchumi, kwa kutoa fursa za ajira, kurahia shughuli za kiuchumi na mafanikio haya yamekuwa muhimu kwetu kama taasisi ya kifedha kwa kutoa fursa kwetu kuhudumia kundi kubwa la wanamichezo na wadau wa sekta hii muhimu,’’ alisema Masuke.
Naye Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura alisema: “Imekuwa ni bora zaidi kwetu sababu hii ni mara ya kwanza kupata mdhamini mmoja anaweka nguvu kwenye ligi zetu. Umuhimu wa hatua hii unaonekana zaidi katika urahisishaji wa maamuzi muhimu bila uwepo wa miingiliano ambayo muda mwingine ingeweza kutuchelewesha. Tunawashukuru sana NBC kwa kuona umuhimu wa kuchukua mnyororo mzima wa hizi ligi, tukitarajia mafanikio zaidi.”
